Wapalestina wawili wamelivamia sinagogi mjini Jerusalem na kuwashambulia
waumini waliokuwa ndani ya sinagogi hilo. Wapalestina hao wametumia
bunduki na mashoka katika kisa hicho kilichosababisha vifo vya watu
wanne.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameyataja mashambulizi
hayo ambayo ni ya kwanza kabisa ya umwagikaji damu kuwahi kutokea katika
kipindi cha miaka mingi mjini Jerusalem kuwa kitendo cha wazi cha
ugaidi na unyama usiokuwa na huruma pamoja na ghasia.Kerry amewataka viongozi wa Palestina kukilaani kitendo hicho kwa sauti kali na hasa baada ya kufikiwa makubaliano kadhaa kuhusu msikiti wa al Aqsa, huku akilaumu kwamba kimesababishwa na miito ya uchochezi iliyotolewa na wapalestina ya kuitisha siku kadhaa za kulipiza kisasi.
''Kuwepo kwa matukio kama haya ambayo ni wazi kabisa yanasababishwa na uchochezi wa kuitisha ulipizaji kisasi,bila shaka ni ukosefu wa uwajibikaji na hilo halikubaliki''
Aidha Kerry ambaye amezungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu punde baada ya tukio hilo amewataka viongozi wa palestina kuchukua hatua madhubuti kuzuia kauli za uchochezi.
Israel imesema itachukua hatua kali dhidi ya kitendo hicho kilichoushtuwa umma wa waisraeli huku waziri wa mambo ya ndani nchini humo Yitzhak Aharovovich akikinyoosha kidole cha lawama kwa kiongozi wa wapalestina Mahamoud Abbas pamoja na kundi la Hamas.
''Narudia tena kusema kwamba tutaendelea kutoa usalama kamili katika mji wa Jerusalme na kwa wakaazi wake. Shambulizi la aina hii linaturejesha kwenye ugaidi wanaoupanga kutokana na kauli za wazi za uchochezi ambazo tunazifahamu zinaendelea kutolewa kupitia mitandao,televisheni,redio na maeneo mengine mengi katika mamlaka ya wapalestina inayoongozwa na rais Mahmoud Abbas,na dhamana kubwa tunambebesha yeye,kundi la hamas na kundi la kiislamu la Kaskazini''
Ghasia mjini Jerusalem ,maeneo ya ya Israel na katika maeneo ya wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel zimeongezeka katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita zikichochewa na mvutano juu eneo takatifu la msikiti al Aqsa,na kuzusha wasiwasi wa kuibuka machafuko ya kidini.Polisi ya Israel imesema mashambulizi ya leo yamefanywa na mtu na binamu yake wanaotokea mashariki mwa Jerusalem.
Hamas yapongeza mashambulizi yaliofanyika Jerusalem
Kundi la Hamas kwa upande mwingine limejitokeza na kukipongeza kitendo hicho ingawa limejizuia kusema ikiwa linahusika.
Ikumbukwe kwamba hapo jana dereva wa basi wa kipalestina alikutwa amenyongwa ndani ya gari mjini Jerusalem ambapo kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa maiti uliofanywa na polisi ya Israel umeonyesha alijiua lakini wapalestina wanahisi vingine,Ammar Hajaz ni afisa katika wizara ya mambo ya nje ya Palestina.
''Mpango umeshaandaliwa na utawala wa Israeli pamoja na walowezi wa kiyahudi wanaofanya vurugu kuwashambulia wapalestina na maeneo ya kidini katika Jerusalem kwa kipindi kadhaa sasa,na sisi tumekuwa tukiuonya utawala wa Israel juu ya vitendo hivi''
Ikumbukwe kwamba Shambulizi dhidi ya Sinagogi la wayahudi ndilo la baya kabisa kutokea Jerusalem tangu mwaka 2008 wakati wapalestina walipowapiga risasi waisraeli wanane katika shule ya kidini mjini humo.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !